MTAZAMO WA MWANAMGAMBO : Kati ya Radio na Mashabiki nani Anamua Wimbo Unavuma?

0

 Je ni kweli kwamba nguvu za mashabiki katika kuamua msanii gani ana “hit” / anatoka katika mziki wa kizazi kipya imepungua?

Je, nani ana usemi mkubwa katika “game” ya sasa? Mashabiki ama vyombo vya habari?

Ni swali ambalo nimekumbana nalo mara nyingi ninapoketi na wasanii tofuati tukibadilishana mawazo kuhusu maswala tofauti yanayohusu tasnia yetu ya mziki wa kizazi kipya kanda ya pwani.

Kwa mtazamo wangu, kinyume na dhana inayojengwa na watangazaji wengi kwamba mashabiki ndio huamua wimbo gani una “hit”, mimi naona vyombo vya habari ndivyo vyenye na nafasi kubwa na usemi zaidi linapokuja swala la kushurutisha wimbo unaotamba na kupendwa mashinani.

Nimejaribu kuujenga mtazamo wangu na hoja nne zenye ushahidi na mifano hai katika mpangilio wa tasnia yetu kwa sasa.

  1. NGUVU ZA KUCHAGUA AJENDA.

Kuna nadharia moja maarufu katika ulimwengu wa habari na mawasiliano inayozungumzia nguvu za vyombo vya habari kuchagua ajenda katika gumzo la jamii. Nadharia hii maarufu huitwa “Agenda Setting Theory”.

Nadharia hii ilivumbuliwa na jamaa wawili Max McCombs na Donald Shaw katika utafiti uliozunguka uchaguzi wa mwaka 1968 nchini Marekani.

Nadharia hii inahoji kuwa vyombo vya habari huathiri matazamo wa jamii katika kuamini lipi swala nyeti  na la muhimu katika jamii. Max McCombs na Donald Shaw waligundua kuwa raia waliamini sana maswala yanayogonga vichwa vya habari kuwa ndio maswala muhimu kwa kipindi kile katika jamii yao, jambo lililovipa nguvu vyombo vya habari kuamua swala gani linakua gumzo katika maskani vijijini.

Waandishi katika vitabu Eaton, 1989; Heeter, Brown, Soffin, Stanley & Salwen, 1989; Hill, 1985; McCombs & Shaw, 1972; Roberts, 1992; Rogers & Dearing, 1988; Rogers, et al., 1993 wamethibitisha kwamba maoni ya wanaohojiwa katika utafiti wa kutathmini swala gani ni muhimu katika jamii katika kipindi flani, hufanana na yale yanayoangaziwa zaidi katika vyombo vya habari katika kipindi kile.

Sasa nadharia hii ya Agenda setting imethibitishwa kujitokeza katika vituo vya radio na playlists zao linapokuja swala la kugundua wimbo gani ni bora unaopendwa na kuzungumzia na wengi mashinani. Radio zinapoamua wimbo ni mzuri hakuna nguvu za kupinga kutoka upande wa wasikilizaji.

Hii ni moja wapo ya sababu ninazonifanya kushikilia kwamba vituo vya radio bado vina nafasi kubwa katika kuamua ni wimbo gani unavuma zaidi katika jamii.

  1. USISTIZAJI

Vyombo vya habari hususan vituo vya radio vina uwezo wa kusistiza taarifa moja kusikika mara nyingi.

Hii ni kulingana na waandishi (Behr & Iyengar, 1985), (Wanta, 1988), na (Gitlin, 1980; Iyengar & Kinder, 1987).

Waandishi hawa kupitia vitabu vyao vya utafiti wamehoji kua uwezo huu wa vyombo vya habari kurudia taarifa mara kadhaa huvipa nguvu za  kusistiza taarifa moja na kuipatia umuhimu. Aidha kulingana na mwandishi (Reese, 1991) kurudiwa kwa taarifa moja huvipatia vyombo vya habari uwezo wa kushinikiza na kujenga taswira flani katika jamii.

Linapokuja swala la mziki, vyombo vya habari bado vina nguvu ya kurudia wimbo mara inazopenda na kuufanya wimbo ule kuaminika kuwa mzuri na ulio bora kulingana na viwango vya jamii. Hatua ya kurudia na kuucheza wimbo kila mara humbadilisha msikilizaji na kumfanya kuamini kwamba wimbo unaochezwa mara nyingi ni bora zaidi ya nyimbo zengine zilizowasilishwa, na kupa thamani katika soko la mziki na katika jamii.

Hii ni sababu nyengine inayojenga hoja na mtazamo kwamba vituo vya radio vina nafasi kubwa katika uamuzi wa ni wimbo gani unavuma zaidi katika jamii.

  1. UCHUJAJI.

Vituo vingi vya radio huwasilisha nyimbo mpya kwa wasikilizaji kupitia mfumo sawia na unaotumika na wahariri katika meza za habari, kuwasilisha habari na taarifa mpya kwa wasikilizaji.

Kulingana na mwanasaiokolojia Kurt Lewin aliyevumbua nadharia ya Gate Keeping mwaka wa 1943, wahariri katika meza za habari hupokea taarifa nyingi kutoka kwa maripota wao mashinani, lakini huchuja taarifa na kuchagua kadhaa tu “wanazoona” zinafaa kwenda hewani ama kusomwa kwa waskilizaji, huku zilizosalia zikiuliwa.

Kulingana na Rothenbuhler’s (1985) na Kelliher’s (1981) waliofanya utafiti wa utumikaji wa nadharia hii katika mziki, wakurugenzi wa mziki katika vituo vya radio pia wamepewa mamlaka sawia na yale ya wahariri, kwani wao ndio huamua ni nyimbo gani zitaskika katika playlists za vituo.

Nadharia ya GateKeeping katika swala la mziki hujitokeza wakati ma’producer na wasanii wanapowasilisha kazi zao mpya kwa vituo vya radio na wakurugenzi wa mziki huketi chini na kuamua nyimbo zipi zitaskika na zipi hazitasikika, kulingana na “viwango” vyao.

Ukosefu wa mchango wa wasikilizaji katika kuamua wimbo gani unakubaliwa ama kukatiliwa kuingia katika playlist za vituo vya habari unapatia vituo vya habari mamlaka makubwa katika kuamua ni wimbo gani unavuma katika jamii.

Kulingana na McCombs & Shaw (1972) kuna wakati wasikilizaji wa radio husikiliza radio kufahamu na kugundua ni wimbo gani ni mpya mzuri ulitoka kama vile vile ambavyo wasikilizaji wengine hufungua radio masaa flani, kufahamu matukio yaliyojiri katika ulimwengu wa habari.

Hii ni sababu nyengine inayonifanya kushikilia kwamba vituo vya radio bado vina nafasi kubwa katika kuamua ni wimbo gani unavuma zaidi katika jamii.

  1. USHAHIDI WA UTAFITI.

Dhana kwamba vituo vya radio vina usemi mkubwa katika kujenga umaarufu wa wimbo si geni katika ulimwengu wa wasomi wa maswala ya mawasiliano ya habari.

Waandishi Baldwin & Mizerski, 1985; Breen, 1991; Kinosian, 1995; Kojan, 1993; Maxwell, 1995; Novia, 1995, Smith, 1989 wote wamewasilisha ushahidi wa utafiti kujenga hoja na nadharia mbali mbali kuhusu mtazamo huu.

Aidha vitabu vya awali kama The Psychology of Radio (Cantril & Allport, 1935) na The People Look at Radio (Lazarsfeld & Field, 1946) vimewasilisha ushahidi wa uliotafitiwa kwamba wimbo unapochezwa katika radio unauwezekano mkubwa wa kuwa maarufu zaidi katika soko la mziki.

Kulingana na Rich (1990) na Keith (1991), utafiti endelevu bado umethibitisha na kujenga zaidi mtazamo kwamba radio hufanya wimbo kujizolea umaarufu katika kipindi kifupi.

Hii ni sababu nyengine inayojenga hoja na mtazamo wangu kwamba vituo vya radio vina nafasi kubwa katika uamuzi wa ni wimbo gani unavuma zaidi katika jamii.

 

 

 

Comments

comments

About author

Teddy Mwanamgambo

Teddy Mwanamgambo is an On Air Personality/Producer @ Radio Kaya (93.1FmMsa,94.9FmVoi,99.7FmMlnd) Coast Kenya.

No comments

Skip to toolbar